Saturday, September 28, 2013

JK: Nitaliamrisha JWTZ kupambana na majangili


28th September 2013

Chapa
Rais Jakaya Kikwete
 Rais Jakaya Kikwete amesema ataliamrisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuongoza mapambano dhidi ya ujangili wa tembo, faru na ukataji haramu wa miti kwa shughuli za biashara ambao umefikia kiwango kikubwa Tanzania.

Aidha, amesema sekta ya utalii Tanzania imeanza kutishiwa na uuaji wa wanyama hao na biashara haramu ya meno ya tembo, faru na kuwa tishio hilo litaathiri sekta ya utalii inayochangia asilimia 17 katika mapato ya Taifa na ajira ya watu 300,000.

Rais Kikwete alitangaza uamuzi huo juzi alipozungumza kwenye Mkutano wa Viongozi wa nchi na Serikali kuhusu biashara haramu ya wanyama na bidhaa zake pamoja na biashara haramu ya bidhaa za miti na mbao.

Aliuambia Mkutano huo ulioandaliwa na Rais Ali Omar Bongo Ondimba wa Gabon na Serikali ya Ujerumani kwenye Makao Makao ya Umoja wa Mataifa, kuwa mwaka 1960, Tanzania ilikuwa na idadi ya tembo 350,000 lakini kutokana na ujangili, idadi hiyo ilishuka hadi 110,000 mwaka 2009.

Kuhusu faru, Rais Kikwete alisema kuwa mwaka 1974 walikuwepo 700 Tanzania na sasa wako chini ya 100 kwa sababu ya vitendo vya kijangili.

“Katika miaka ya 1980 na 1990 wakati wa kilele cha ujangili katika mikonga ya wanyama, tulilazimika kutumia jeshi kutuliza hali hiyo. Tuliona matokea mazuri na tulikuwa na utulivu wa aina fulani. Lakini katika miaka minne iliyopita, tumeshuhudia kuongezeka kwa vitendo vya ujangili kwa ari na kasi mpya. Kwa mfano kati ya mwaka 2010 na Julai, mwaka, 2013, zaidi ya tembo 1,386 waliuawa katika Tanzania”.

“Tumechukua hatua kali za kupambana na ujangili ikiwa ni pamoja na sera, sheria na kanuni za kupambana na ujangili. Aidha, tumetia saini mikataba mbalimbali ya kimataifa ya kupambana na ujangili huu”, alisema.
Aliongeza kuwa kati ya mwaka 2010 hadi katikati ya mwaka huu, 2013, jumla ya majangili 5,189 wametiwa mbaroni na silaha 1,952 zimekamatwa.

Aidha, vipande 3,788 vya meno ya tembo vimekamatwa vikiwa na uzito wa kilo 10,756 vilikamatwa nchini.
“Nimeamuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania kukabiliana na hali hiyo na naamini kuwa tutapata mafanikio makubwa zaidi katika operesheni inayoandaliwa”. alisisitiza.

Hata hivyo, Rais Kikwete alisema kuwa bado shughuli za kupambana na ujangili, zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na mahitaji ya watumishi 4,800 wapya kwa ajili ya kupambana na ujangili hata kama wameajiriwa wafanyakazi 500 tu mwaka huu.

“Pamoja na kwamba tuna matatizo ya watumishi, bado pia tuna matatizo ya raslimali fedha. Bajeti ya sasa ya dola za Marekani 6.9 milioni kwa ajili ya Idara ya Wanyamapori haitoshi kutimiza yote haya. Tunahitaji dola za Marekani milioni 19.4 kwa ajili ya shughuli hiyo na nyongeza ya dola milioni 30 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi. Tukiachiwa pekee yetu hatuna uwezo. Tunaomba twende pamoja katika hili”, alisema.
CHANZO: NIPASHE